Monday 18 April 2016

Waajiri wanatarajia nini kwa waombaji wa kazi?

Taarifa ya Utafiti wa Ajira na Kipato ya mwaka 2012, iliyotolewa na Idara ya Takwimu ya Taifa mwezi Julai 2013, inaonyesha kwamba nchi yetu ina waajiriwa rasmi 1,550,018.  Kati yao asilimia 64.2 wameajiriwa katika sekta binafsi na walibaki (asilimia 35.8) wameajiriwa katika sekta ya umma. Hata hivyo, taarifa inasema ni asilimia 24.8 pekee ya wafanyakazi hawa, wanapata kipato cha kuanzia Tsh 500,001 na kuendelea kwa mwezi [vipato vya wafanyakazi wengi (asilimia 54.4) ni chini ya Tsh 300,000 kwa mwezi.]

Nafasi za kazi zisizoweza kujazwa na watafuta kazi wasiopata kazi

Taarifa hiyo imejaa takwimu zinazothibitisha kwamba soko la ajira hapa nchini linakabiliwa na changamoto kubwa. Kwa mfano, wakati kwa mwaka 2011/12 kulikuwa na nafasi za kazi 126,073, ni wafanyakazi wapya 74,474 tu waliingia kwenye soko la ajira kwa kipindi hicho. Takwimu nyingine za Wizara ya Kazi na Ajira zinaonyesha kwamba nafasi za kazi zipatazo 45,388 hazikuweza kujazwa katika kipindi hicho.

Pamoja na ukweli kwamba uwezo wa waajiri kuajiri wafanyakazi wapya unategemea sana fedha na maandalizi mengine muhimu, lakini upo ukweli kwamba watafuta kazi wengi hawakuwa na sifa zinazotakiwa na waajiri ikiwemo uzoefu.

Katika kulithibitisha hilo, Baraza la Shirikisho la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) kwa ushirikiano na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) lilifanya utafiti kujua mitazamo ya waajiri kuhusu wahitimu wa vyuo vikuu. Matokeo yalionyesha kuwa waajiri hawana imani na weledi wala ujuzi wa wahitimu hawa na kwamba zaidi ya nusu ya watafuta kazi wenye shahada, hawana sifa za kuwawezesha kuajirika. Tanzania, kwa mfano ina asilimia 39 tu ya wahitimu ya vyuo vikuu wenye ujuzi unaokidhi vigezo vinavyohitajika na wajiri wao. 

Kwa matokeo hayo, inavyoonekana, mbali na ukosefu wa ajira, nchi yetu inakabiliwa na tatizo kubwa la watu wanaotafuta kazi, kwa maana ya kuamini wanazo sifa, lakini kwa upande mwingine, hawaajiriki hata kama kazi hizo zipo. Lakini ieleweke kwamba hapa tunazungumzia kazi zinazohitaji ujuzi wa kusomea.

Kwa upande mwingine, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, katika watu wenye uwezo wa kufanya kazi zozote hata zile zisizohitaji ujuzi rasmi na wanaofanya kazi, watu wapatao 2,409,862 wanafanya kazi chini ya uwezo wao (under-employed) katika nchi hii. Hiyo ikiwa na maana kwamba watu wengi wanapoteza muda makazini na hufanya kazi kwa kiwango kidogo mno kuliko ilivyowapasa kufanya.

Ukosefu wa kazi ni pamoja na kutokuajirika

Kwa kawaida imezoeleka kwamba ukosefu wa kazi hutokea katika mazingira ambayo mtu anayeamini kuwa anazo sifa za kuajiriwa, na anayetafuta kazi, anashindwa kupata kazi hiyo. Kwa mfano, mhitimu wa sayansi ya siasa, mwenye ufaulu mzuri na mwenye nia ya kuajiriwa, anaposhindwa kuajiriwa, tunaweza kusema kwamba mhitimu huyo anakabiliwa na tatizo la ukosefu wa kazi.
Wahitimu wenye matumaini makubwa ya kuingia kwenye soko la ajira. Si mara zote furaha hii hudumu. Picha: @Michael


Hata hivyo, mtu anayetafuta kazi na hapati, bado anaweza kuwa na sifa za kuajirika, kwa maana ya kuwa na ujuzi, uelewa na sifa zinazomfanya awe katika nafasi ya kuajiriwa kirahisi na zaidi ya hayo, kuwa na uwezo wa kufanikiwa katika ajira hiyo kwa maana ya kujinufaisha mwenyewe, mwajiri wake, jamii na uchumi kwa ujumla, ingawa anaweza kuwa hana kazi.

Mtu asiyeajirika, ni yule ambaye, mbali ya kutokuwa na kazi au kushindwa kupata ajira, hana ujuzi wa kiutendaji anaopaswa kuuonyesha kwa mwajiri ili si tu aweze kupata kazi, bali adumu katika kazi hiyo kwa muda mrefu (ikiwa atapenda) bila hofu ya kuikosa kazi hiyo. Kwa maneno mengine, mtu asiyeajirika, anaweza kuwa na kazi, lakini hawezi kujihakikishia kazi hiyo kwa muda mrefu na hana uwezo wa kuhama kutoka kazi moja kwenda kazi nyingine sawa na mahitaji yake.

Katika mazingira ambayo asilimia 64.2 wameajiriwa katika sekta binafsi, ambazo mara nyingi huwa ni ajira za muda/mkataba, unaweza kuona athari za kuwa na watu ambao, kwanza hawana ujuzi unaowawezesha kupata kazi, lakini pia hawawezi kuonyesha weledi na ufanisi kazini, na hivyo wanakuwa katika hatari ya kukosa ajira katika kipindi ambacho wangependa kuendelea na ajira hizo.

Mwajiri hutafuta nini anapoajiri?

Tafiti nyingi za kazi na ajira zinaonyesha kwamba pamoja na umuhimu wa kuwa na cheti chenye alama za juu, waajiri wengi hawana uhitaji sana na alama nzuri. Badala yake, wengi wao huhitaji kuona ujuzi na weledi kazini unaotafsika kwa uwezo wa kutumia maarifa na uelewa wa darasani katika kutatua changamoto za kazi.

Kwa maana nyingine, mwajiri anakutarajia uwe na uwezo wa kuhusisha na kuzitumia nadharia, maarifa na kanuni za kitaaluma katika kufumbua matatizo ofisini kwake ukikumbuka kwamba ufanisi wa kazi, mara nyingi hautegemei nadharia ulizozitumia kufaulu mitihani.

Ni wazi kwamba mwajiri anahitaji ujuzi rahisi (soft skills) ambao kimsingi husaidia kuongeza ufanisi kazini. Ujuzi huu mwepesi hupatikana kwa jitihada binafsi nje ya mfumo rasmi wa kitaaluma. Mfano ni uwezo wa kujiamini kuwa unaweza (efficacy) na kujitambua kazini, ujuzi wa kihaiba kama vile kuzingatia muda na hata kufanya na kumaliza majukumu ndani ya muda uliopangwa. Utakubaliana nami kwamba mtu asiye na tabia ya kuzingatia muda katika kazi, thamani yake hupungua hata anapokuwa na ujuzi wa kazi.

Mfano mwingine wa ujuzi rahisi ni mahusiano bora ya kikazi na watu wengine katika kuongeza ufanisi. Utakubaliana nami kwamba kazi hufanyika kwa ushirikiano na wengine. Bila mahusiano mazuri na wengine, pengine kwa ile hulka ya kupenda kuwazidi wengine, ufanisi wa kazi kwa pamoja unaweza kuathirika. Mwajiri asingependa hili litokee.

Lakini pia kuna vitu vidogo-vidogo kama vile matumizi sahihi ya lugha, mpangilio wa kazi na kadhalika. Ni fedheha kwa mfano, unapokuwa Injinia mwenye uwezo wa juu katika uinjinia, lakini huwezi kuongea kwa ufasaha unapolazimika kufanya hivyo. Fikiria unapokuwa mfanyakazi mzuri mwenye ujuzi wa kazi lakini huwezi kuandika barua inayoeleweka. Ni fedheha ambayo si waajiri wengi wanaweza kuivumilia.

Kadhalika, ubunifu ni alama muhimu anayoihitaji mwajiri. Ni namna mwajiriwa anavyoweza kutumia raslimali chache zizizopo ili kuleta matokeo yanayozidi matarajio. Ni uwezo wa kuinufaisha taasisi kwa werevu, ujuzi na maarifa binafsi ambayo wakati mwingine hayakutarajiwa na wengi.

Vile vile, uzoefu ni hitaji la msingi kwa waajiri wengi. Ni kweli kwamba kwa haraka unaweza kudhani hiki chaweza kuwa ni kikwazo kwa watafuta kazi wengi. Lakini ni dhahiri pia kwamba mwajiri yeyote angependa kuona uthibitisho dhahiri kwamba mwombaji wa kazi au mwajiriwa anao uwezo wa kumudu majukumu anayoyaomba kwake au aliyoyakabidhiwa.

Uzoefu huu unaweza kupatikana kupita kazi ulizopata kuzifanya kabla ya ajira husika iwe kwa ajira rasmi au kwa kujitolea. Ni kwa mantiki hiyo unashauriwa kutafuta fursa za kujitolea kufanya kazi zinazofanana na ajira unayoitamani wakati ukiendelea na masomo au ukisubiri kuajiriwa.

Zaidi, mwajiri huvutiwa kuona uwezo wa kiuongozi kwa mwajiriwa tarajali au mwajiriwa aliye kazini. Sasa tunapozungumzia uongozi hatumaanishi madaraka. Madaraka na uongozi si lazima vimaanishe dhana ile ile. Hapa tunazungumzia uwezo wa kuwaonyesha njia na kuwahamasisha wengine kufikia malengo mapana ya kazi.

Uongozi ni namna mwajiriwa anavyoweza kufanya maamuzi sahihi kwa wakati akishirikiana na wengine pasipo kusimamiwa kwa karibu na wakubwa wa kazi. Uongozi ni pamoja na namna mwajiriwa anavyoweza kufanya majukumu mengine kwa moyo wa hiari na kujituma ili kufikia malengo mapana ya taasisi ni sehemu ya uongozi. Uongozi ni sifa muhimu ambayo si lazima uisomee darasani lakini inayotarajiwa na waajiri wengi.

Hitimisho

Kwa kuhitimisha tunaweza kusema, pamoja na ukweli kwamba nchi yetu inakabiliwa na ukosefu wa ajira, bado, kuna ukweli kwamba waajiriwa wengi hawaajiriki kwa maana ya kukosa weledi na ujuzi unaotakikana na waajiri ili kuweza kuajiriwa na pia kudumu katika ajira zao. Ingawa ni kweli kwamba tunayoyasoma madarasani yana nafasi kubwa ya kuamua wapi tuajiriwe, lakini ni kweli pia kwamba upo ujuzi muhimu tunaouhitaji usiohotaji sana vyeti tulivyo navyo.

Yote haya ni rahisi kuonekana kupitia barua ya maombi ya kazi na maelezo binafsi anayoandika mwombaji wa kazi na hata anapokuwa anatekeleza majukumu yake kazini kama mwajiriwa tarajali. Katika makala zijazo, tutazungumzia kile kinachoweza kufanyika katika kuwasaidia watafuta kazi kujiongezea ujuzi huu tulioupitia hapa kwa haraka na, kadhalika, namna ya kuandika barua na maelezo binafsi (wasifu) yanayoonyesha haya tuliyoyajadili kwa kifupi.

No comments:

Post a Comment