Thursday 21 April 2016

Fahamu haki na wajibu wa mfanyakazi kisheria

Huwezi kudai kitu ambacho hufahamu kuwa kipo na hata kama unajua kipo hujui kinapatikanaje na hata kama unajua kinavyopatikana hujui nani anawajibika kukupatia.
Kama kuna jambo la muhimu kwa mfanyakazi, kabla ya kazi yenyewe na mshahara atakaolipwa ni kujua haki zake na wajibu wake kisheria.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004, kanuni za ajira na uhusiano kazini za Mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi ya Mwaka 2003 na marekebisho yake; mfanyakazi anazo haki nyingi ambazo anapaswa kuzifahamu na kuzipata.
Haki hizi ni pamoja na kupatiwa mkataba wa kazi, kufahamu ameajiriwa katika nafasi gani na majukumu yake yatakuwa ni yapi, ili asije akafanya majukumu yasiyomhusu. Mfanyakazi ana haki ya kwenda likizo (siku 28) ndani ya kila mzunguko wa miezi 12, kupatiwa likizo ya matibabu (siku 126) endapo ataugua. Likizo ya uzazi ambayo kwa mwanamke ni siku 84 kwa mtoto 1 na siku 100 kwa mtoto zaidi ya 1. Mwanamume likizo ya uzazi ni siku 3.
Mfanyakazi ana haki ya kulipwa malipo stahiki yanayoendana na kazi anayofanya na kiwango kilichowekwa na Serikali kwa mujibu wa sheria. Hii ni pamoja na malipo ya muda wa ziada.
Endapo mfanyakazi ataumia akiwa kazini ana haki ya kuhudumiwa kwa matibabu na mwajiri pamoja na kulipwa fidia ya madhara aliyoyapata. Mfanyakazi ana haki ya kupatiwa vitendea kazi na mazingira rafiki ya kufanyia kazi siyo hatarishi. Kutobaguliwa, kutonyanyaswa, kutonyanyapaliwa, kutotengwa, kutodhalilishwa kijinsia na kutopigwa ni mojawapo ya haki za mfanyakazi. Mfanyakazi yuko huru kujiunga na chama cha wafanyakazi.
Mfanyakazi ana haki ya kuvunja mkataba wa kazi kwa kufuata utaratibu uliowekwa kisheria. Endapo mfanyakazi ataachishwa kazi au kustaafishwa, anaweza kuwa na haki ya kulipwa malipo ya notisi, kiinua mgongo, usafiri, cheti cha utumishi, mafao ya hifadhi ya jamii, malimbikizo ya likizo na malipo mengineyo. Mfanyakazi pia ana haki ya kugoma baada ya kufuata utaratibu wa kisheria, ili kushinikiza madai yake kutekelezwa au ili kufikisha ujumbe kwa mwajiri.
Sheria pia imeweka wazi wajibu wa mfanyakazi kuwa ni pamoja na kufanya kazi kwa bidii, kufikia malengo ya mwajiri, usiri, utii, nidhamu na uaminifu. Kutoa taarifa kwa maandishi mapema tatizo linapotokea wakati wa ugonjwa, ajali au kuibiwa.
Kutoa notisi au malipo unapotaka kuacha kazi, kutoa taarifa ya kujifungua kabla ya mwezi husika, kuwa mbunifu na kulinda masilahi ya mwajiri wakati wote, kufuata utaratibu za kisheria wakati wa migomo na kutumia njia za kidiplomasia kutatua migogoro na mwajiri badala ya njia za uvunjifu wa amani. Kumbuka kila haki inaambatana na wajibu. Kabla hujadai haki zako timiza kwanza wajibu wako. Pia, wakati mwingine haki haipatikani kirahisi, kwa nidhamu ya woga au kwa maneno pekee. Kuwa jasiri, jenga hoja, dai haki zako kwa kufuata utaratibu na sheria ya kazi.
-

No comments:

Post a Comment