Katika
kutafuta
ajira, kama ilivyo katika shughuli nyingine, kuna kanuni. Hebu
tuchukulie wewe ni kijana na ndiyo kwanza umemaliza masomo yako
ya chuo na umeenda kwenye usaili (Interview) kwa ajiri ya kupata ajira.
Unafikiri hasa ni mambo gani ambayo unatakiwa kufanya?
Hebu
tuanze na kujiamini. Hakuna kitu utakachosema wakati wa usaili kinachoweza kuwa
na umuhimu kama mwenyewe hutaonekana mtu mwenye kuaminika. Kiongozi wako mpya
wa kazi ni lazima akuamini. Hakuna mtu aliyetayari kuajiri mtu ambaye anajua
hatomwamini. Sasa ni vipi utajenga kuaminika?
Kwanza
ni muhimu uzungumze ukweli. Wapo watu wenye uwezo wa kuongopa vizuri sana na
wasigundulike. Lakini hawa ni wachache sana. Wengi wetu huweza kujikuta
tukigundulika kwamba hatusemi ukweli.
Unajua
jinsi ambavyo hata wewe mwenyewe umewahi kuzungumza na mtu na kuhisi kwamba
anachokueleza si ukweli. Hilo ni tatizo la wengi wetu na wala usidhani ni
tatizo la huyu mtu aliyekuwa akikueleza wewe tu.
Kama
unajiamini na unaamini ukweli wa kile unachosema. Hata uwe mtu mwenye tabia ya
wasiwasi kiasi gani, hali ya uwazi na usahihi wa mazungumzo yako itaonekana
wazi.
Pili,
unatakiwa kuwatazama machoni unaozungumza nao. Huna haja ya kuishangaa miguu
yao, ama kushangaa kikombe kilichowekewa kalamu juu ya meza ya msaili wako au
kushangaa feni iliyo kwenye dari la chumba cha usaili
Fanya
kila jitihada umtazame moja kwa moja msaili au wasaili na uzungumze katika hali
ya kawaida iwezekanavyo. Hakutakuwa na
tatizo kuwatazama machoni wakati unapeana mikono na kuwaeleza, ‘samahani,
kidogo mimi mimi nina tatizo la kukumbwa na wasiwasi kirahisi’. Kama ni msaili
au wasaili ni wenye busara, ni lazima watazungumza kitu chenye lengo la kukutoa
wasiwasi.
Lakini
ikiwa msaili ataonesha kukudharau kwa kauli yako hiyo ya ukweli, basi kuwa na uhakika
kwamba hata ukipata nafasi unayotaka hutofurahia kufanya naye kazi.
Unataka
kumvutia mkuu wako mtarajiwa wa kazi pamoja na wafanyakazi wenzako, kama vile
wewe unavyopenda majukumu yako. Hivyo, kuwa wazi na mwaminifu katika kipindi
chote cha usaili, na kumbuka kwamba unayo nafasi ya kuwasaili wao pia kama
wakuu wako wa baadaye wa kazi, na wala si jambo la upande mmoja. Kama ilivyo
kwako, nawe unatakiwa kuwa na hakika kama utafanya nao kazi vizuri.
Hebu
sasa tutazame picha kwa ujumla ya namna unavyoweza kujtafutia soko na
kujitambulisha kama mtu mwenye uwezo wa kazi, mwenye uwezo wa kutegemewa,
mwenye akili, mwaminifu na rasilimali nzuri za baadaye kwa kampuni.
Kwanza,
huwezi kuanza kuomba kazi, bila kujiamini kwamba una vitu vyote hivyo. Mkesha wa
siku ya usaili, pitia mambo yote muhimu ambayo mkuu wako wa kazi angepennda uwe
nayo kama mfanya kazi wake.
Chukua
nafasi ya mkuu wako huyo wa kazi akilini mwako na ufikirie kama ungekuwa wewe
ni vitu gani ungetafuta kama mfanyakazi wako mpya. Unaweza kufanya majaribio ya
usaili na ukiweza, mpate rafiki yako atakayekusaidia kufanya hivyo.
Unaweza
kujiuliza maswali yafuatayo…Nina uwezo? Ninao utaalamu wa msingi unaotakiwa ili
kuweza kuifanya kazi hii ama nahitaji mafunzo zaidi? Ni vipi nitaweza kujifunza
kwa haraka.
Haitakuwa
vibaya sana kwako kama ukienda zaidi ya uwezo wako wa sasa na kujaribu kutazama
mambo yanayoweza kuwa changamoto. Lakini unatakiwa kuwa mwaminifu na huna haja
ya kujidai tayari unaweza kila kitu, kwa kiwango cha juu kabisa, wakati una
hakika si hivyo.
Endelea
na orodha ya maswali…Je wewe ni mtu wa kutumainiwa? Ni uwezo upi mpya mbali na
yale uliyoorodhesha kwenye orodha ya mahitaji ya kazi utakaouleta kwenye
kampuni? Uwe tayari kumweleza msaili wako mambo ya ziada ambayo kampuni
itafaidika nayo ikiwa itakuajiri.
Rudia
majibu yajo kwa msaili wako wa kufikirika, ili utakapoingia kwenye chumba cha
usaili uwe tayari na mawazo ya kile utakachomweleza msaili wako ili kujitafutia
soko vizuri.
Kwa kuwa
na majibu yako yaliyotayarishwa, utakuwa na wakati rahisi wa kujitambulisha
kama mtu mwenye busara na akili hata kama una kawaida ya kuogopa sana pale
usaili wa kweli unapoanza.
Mwisho,
usijaribu hata siku moja kuonyesha kutokujiamini. Wahi muda uliopangwa, vaa
nguo zinazohitajika kwa ajili ya kazi uliyoomba, jua jina la kampuni unayoomba
kazi, kazi unayoomba, na mfahamu anayekusaili.
Ni vema
ukawahi na kujua zilipo huduma nyingine za muhimu kama choo, bafu na kadhalika.
Huna haja ya kulijaza tumbo lako na vitu vya majimaj ama chakula.
Baadhi
ya mambo haya yaweza kuonekana ya kijinga, lakini hakuna kitu kibaya kama
kuonekana ukihangaika kwenye kiti ulichoketi kutokana na usumbufu wa tumbo ama
kibofu chako cha mkojo, wakati unatakiwa kuonekana mwenye kujiamini, uliyetulia
na uliyetayari kwa usaili.
Kuwa
macho na namna unavyozungumza. Epuka kutumia maneno makali na lugha ya mtaani. Kuwa
macho na lafudhi. Usiruhusu lafudhi ya ajabu au sauti iliyosikia ikufanye ukose
kazi uliyokuwa ukiitoa siku zote.
Kumtumia
rafiki yako kwa usaili wa majaribio, kwa weza kukusaidia kuongeza sana
kujiamini wakati msaili wako wa kweli atakapokuwa mbele yako. Kama kweli
unajiamini, kujitafutia soko hakuwezi kuwa jambo gumu. Fanya mazoezi kwa kile
unachotaka kukisema.
Kama
kweli hujiamini, basi ni bora ukafanya jitihada za kuondoa tatizo hilo kwanza. Kama
lengo ni kujijengea maisha mazuri na ya furaha, basi iko haja ya wewe nawe
kuwasaili wanaotaka kukuajiri ili kujua kama watafaa kukujengea maisha hayo ya
furaha baadaye. Unatafuta mwajiri aliyetulia na rahisi kufanya naye kazi.
Kwa makala
nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi kila
siku.
Tunakutakia
kila la kheri katika mafanikio ya kazi unayoitafuta.
Ni wako
rafiki katika mafanikio,