Monday 18 April 2016

Maana ya Saikolojia na nafasi yake katika jamii

SAIKOLOJIA, neno lililotoholewa kutoka neno la kiingereza psychology, si elimu inayoeleweka sana katika jamii yetu. Ingawa ni kweli neno hilo, saikolojia, linafahamika kwa wengi, bado yapo mengi yasiyofahamika vyema kuhusu saikolojia. Tunaposikia saikolojia, au mtu anaposema yeye ni mwanasaikolojia, mawazo yetu yanahamia kwenye kitu kinachofanana na uaguzi. Kwamba mwanasaikolojia ni mtu mwenye uwezo wa kusoma mawazo ya mtu bila hata kuongea naye, na tena anao uwezo usio wa kawaida wa kubashiri majibu sahihi ya matatizo yanayomkabili mtu huyo. Kwa hakika, hii ni dhana maarufu lakini isiyo na usahihi wowote.

Katika makala haya, ningependa kusaili kwa ufupi maana ya saikolojia kama taaluma ili kuifanya ieleweke kwa wasomaji ambao ni hakika wanaisikia kwa kiasi kikubwa na kisha nitajaribu kuonyesha nafasi ya taaluma hiyo ngeni katika jamii yetu ambayo yaweza kutumika katika kutatua matatizo ya kijamii na hivyo kuharakisha juhudi za watu kujiletea maendeleo yao.

Saikolojia ni nini?

Neno kuu linalobeba dhana kamili ya saikolojia ni tabia. Saikolojia ni sayansi ya tabia. Tunapozungumzia tabia, tuna maana ya matendo, mienendo au hulka zinazoweza kuonekana wazi, kupimwa na hata kuchunguzika kwa misingi ya kisayansi. Mfano, hasira ni tabia kwa sababu kwanza, ni kitendo kinachoweza kuonekana bayana kwa macho kupitia yanayofanywa na mwenye hasira, na hivyo inaweza kupimwa kisayansi kwa kufuatilia vitendo vinavyoonesha hasira ili kuweza kufanyiwa utafiti unaokubalika. Maelezo hayo hayo yanaweza kutumika kuelezea tabia yoyote kama vile kupenda, kunyanyapaa na kadhalika kwa sababu, vyote kwa pamoja, vinaonekana, vinapimika na vinachunguzika kwa kufuata kanuni za kisayansi.

Kwa nini unaona unachokiona kwenye picha hii? Picha: serc.carleton.edu

Ingawa msingi wa tabia yoyote ni mawazo, imani, fikra, mitazamo isiyoonekana, lakini ni wazi kuwa yote hayo hujidhihirisha kwa yanayoenekana. Hii ndio kusema kwamba yanayoendelea kwenye ufahamu wa mtu (cognition) ambayo ni mkusanyiko wa dhana, maarifa, imani, mitazamo (attitude) aliyonayo mtu huyo, huonekana kwa matendo yanayoonekana bayana kwa jinsi ya tabia. 

Kwa hiyo, tunapozungumzia saikolojia, kimsingi tunazungumzia msingi wa tabia zetu na jinsi tabia hizo zinavyojiumba kwa maana ya namna zinavyoanzia mbali kwenye ufahamu kisha kuhamia kwenye mitazamo ambayo ndiyo huzaa matendo yanayoonekana na ambayo tunayaita tabia.Tabia hii, kama tulivyoona, huchunguzwa kwa kutumia majaribio (experiments) ya kisayansi na wala sio hisia, maoni au bashiri za kimazoea.

Historia na maendeleo ya elimu ya saikolojia

Safari ya maendeleo ya elimu ya saikolojia imetegemea kwa kiasi kikubwa namna tabia inavyotazamwa kwa maana ya chanzo chake na jinsi  inavyoweza kubadilishwa. Wakati Saikolojia inaanza miaka ya nyuma, iliaminika kuwa  ni elimu ya mambo ya nafsi ambayo kwa hakika hayaonekani kwa macho. Hivyo, wanasaikolojia wa mwanzo walitumia muda mwingi kuchunguza nafsi msisitizo ukiwa katika mahusiano ya tabia na nguvu zilizo nje ya uwezo wa mwanadamu kwa kutumia uzoefu. Mfano, ungeenda kwa mwanasaikolojia na akakusaidia kujitambua kwa kutumia ndoto unazoota mara kwa mara.

Waliamini kuwa tabia hujiumba pasipo jitihada za mwanadamu na hivyo mwanadamu hana uwezo wa kudhibiti wala kubadili tabia yake. Kutokana na hayo wanasaikolojia wa mwanzo walijikuta wakifanya shughuli zisizotofautiana sana na falsafa (speculations) na wanajimu kwa sababu ya mbinu zisizo na misingi yoyote kwenye sayansi na utafiti.

Lakini baadae, elimu hii iliendelea kukua na wanasaikolojia wakaanza kuhusisha mazingira anamokulia mtu na tabia yake. Tabia ilichukuliwa kama matokeo ya kujifunza na hivyo ingeweza kudhibitika na hata kubadilishwa. Kujifunza hutokana na ama namna matendo yetu yanavyoleta matokeo chanya au yanayotuathiri ikiwa na maana tabia inayoambatana na matokeo chanya hukua na kuendelea wakati tabia inayoendana na matokeo hasi hufifia na kupotea. Ili kufahamu matokeo ya matendo/tabia fulani, ni lazima tabia hiyo ionekane na ipimike (quantifiable) tofauti na ilivyokuwa katika mtazamo wa awali. Hii ilikuwa ni hatua kubwa katika kuanza kwa tafiti za kisayansi zinazohusu tabia.

Hata hivyo, pamoja na maendeleo hayo, bado yalikuwepo mashaka ya namna mazingira yanaweza kuongoza tabia ya mwanadamu mwenye utashi. Ndipo baadae, saikolojia ikaanza kutazama kwa kina uhusiano wa utashi na mazingira anamokulia mtu katika kujenga tabia. Kwamba pamoja na tabia ya kuathiriwa na mazingira, bado utashi binafsi unaweza kuamua muundo wa tabia husika.

Kwa sasa, mtazamo unaotawala elimu ya saikolojia ni namna utashi, mtazamo na mazingira unavyoathiri tabia na jinsi tabia hali kadhalika inavyoathiri utashi, mtazamo na mazingira ya kijamii. Athari hizo zinazotegemeana kati ya mawazo, uelewa, mitazamo na mazingira ya kijamii huchunguzwa kwa kufuata kanuni za tafiti za kisayansi ambazo mara nyingi hufanyikia maabara.

Nafasi ya saikolojia katika jamii

Matatizo mengi yanayoikabili jamii yetu yana chanzo chake katika tabia. Tabia ndio chanzo cha matendo tunayoyaona kama kukosekana kwa uaminifu, ubadhilifu wa mali za umma, ufisadi, migogoro ya ndoa, misuguano ya kijamii, chuki, upendo, ugaidi, unyanyapaa, ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kidini, changamoto za kimalezi na kadhalika. Yote haya yanaweza kuchambuliwa na kupatiwa majibu yake kwa kutumia sayansi ya tabia. Hapa nitatoa mifano mifano kadhaa kuonyesha namna sayansi ya tabia, inavyoweza kutumika kutatua matatizo yanayoikabili jamii.

Mosi, katika elimu, saikolojia hutumika katika kubaini mahitaji halisi ya mtoto kiufahamu, kijamii, kihisia na kimwili kulingana na umri wake. Kwa kuyaelewa hayo inakuwa nyepesi kubuni mtaala unaokidhi mahitaji hayo kwa ufasaha. Hili limekuwa likifanyika kwa kutumia saikolojia ya elimu katika mafunzo ya ualimu na elimu. Changamoto kubwa imekuwa ni namna walimu wanavyoweza kutafsiri malengo mapana ya mtaala katika kujibu mahitaji halisi ya mtoto.

Kupitia sayansi ya tabia, tunaweza kuelewa namna mwanadamu anavyojifunza, kuelewa na hata kutumia anachokielewa katika kuyaelewa na kuyafanya mazingira yake kuwa bora zaidi. Namna gani mtoto hujifunza lugha, na athari za lugha hiyo katika uelewa wake ni mambo ambayo kupitia saikolojia tunaweza kuyaelewa vizuri.

Kijamii, matatizo ya kimahusiano baina ya watu yanayosababishwa na tofauti za kimtazamo, itikadi, imani na kadhalika yanaweza kuchambuliwa na kutatuliwa kwa kutumia saikolojia. Ilivyo ni kwamba zinapotokea hitilafu za kimahusiano, watu wengi hushindwa kuyatazama mambo kwa macho yasiyo ya upendeleo. Na kwa kawaida watu hukwepa kubeba lawama yanapotokea matatizo na kufanya juhudi za kuwafanya wengine wawajibikie matatizo ambayo wakati mwingine wameyasababisha wao.

Hapa ndipo, washauri nasaha, kwa kutumia saikolojia, wanapoweza kuwa msaada kwa kuwasaidia watu hawa kuelewa mzizi wa matatizo yao na hivyo kukabiliana vyema zaidi na matatizo hayo. Kazi ya mshauri nasaha si kutoa majibu, bali kutumia taarifa za mwenye tatizo katika kumsaidia kutambua kiini cha tatizo ambalo mara nyingi hufunikwa na dalili tu za tatizo. Hivi ndivyo matatizo kama ya msongo wa mawazo, hasira, chuki, unyanyapaa, ubaguzi wa rangi, na mengineyo yanavyoweza kushughulikiwa kwa ushirikiano na washauri nasaha.

Kadhalika, kupitia kanuni za saikolojia, program endelevu za kijamii za kubadili tabia na mitazamo ya watu inayowakwaza katika kuishi maisha yenye ufanisi zinaweza kufanyika ili kuondoa au kupunguza matatizo ya kiafya, kijamii na kiimani. Kwa hakika, kuelewa jambo hakutoshi kubadili tabia ya mtu. Ni lazima zifanyike jitihada za kugeuza mitazamo ili kuweza kubadili tabia za watu.

Vile vile, kuna suala la malezi na makuzi ya mtoto. Ni wazi kwamba wazazi wanakabiliwa na changamoto mpya za kimalezi zinazosababishwa na mabadiliko ya kijamii yanayoendelea. Malezi ya enzi za sasa hayafanani na yale ya miaka ya 90. Ni kweli kuwa kadri mtoto anavyokua kiumri, anakutana na changamoto nyingi ambazo ni vigumu kuzishughulikia  kikamilifu pasipo elimu ya saikolojia ya makuzi. Kwa kupitia elimu hii tunaweza kuwasaidia wazazi kuelewa kwa upana namna njema ya kujibu mahitaji ya watoto wao katika mazingira yanayobadilika kwa kasi na hivyo kuwafanya wakue wakiwa raia wenye mitazamo chanya kwa maisha yao wenyewe na watu wanaowazunguka.

Lipo pia suala la uongozi. Namna gani wanasiasa au viongozi wengine wanaweza kuwashawishi wananchi au watu wanaowaongoza kukubali mawazo yao wakati huo huo wakidhibiti mawazo ya watu wanaofikiri kinyume nao, panahitajika kanuni za saikolojia. Falsafa, mitazamo na imani za kisiasa zinaweza kuwaingia ipasavyo wafuasi wa wanasiasa, na kuwafanya wajipambanue na makundi yao ya kisiasa, kwa kutumia kanuni za kisaikolojia.

Sambamba na hilo, katika biashara na ofisini, unafanyaje kuongeza ari ya wafanyakazi ili waweze kufanya kazi pasipo kusukumwa hata kama huwalipi fedha za kutosha au kama mfanyabiashara anafanya kipi ili kuwavutia wateja kupenda bidhaa yake kupitia matangazo, katika mazingira ambayo biashara ni ushindani, unahitaji ushauri wa kisaikolojia. Unapoona tangazo linalomwonyesha mtu maarufu akitangaza bidhaa fulani, hayo ni matumizi ya saikolojia. Namna gani matangazo yanayolenga kubadili tabia za watu yanavyoweza kuandaliwa, nayo ni kazi ya saikolojia.
 
Katika kuhitimisha  tunaweza kusema ni kweli kwamba saikolojia ni maisha ya kawaida. Huwezi kuhusiana na mtu bila kutumia basics za saikolojia. Hata hivyo, pamoja na kufahamika kijuu juu, bado nafasi ya saikolojia haijaanza kutambulika ipasavyo katika jamii. Bahati mbaya, uelewa potofu wa sayansi ya tabia, yaani saikolojia, ndio unaochukua nafasi na hivyo kuweza kuleta madhara makubwa jamii.

Kwa mfano, ushauri wa kimahusiano unaotolewa kwenye vyombo vingi vya habari, mara nyingi umejikita kwenye uzoefu binafsi anaokuwa nao 'mshauri' husika ambao si lazima ufanye kazi katika mukhtadha (contexts) mwingine. Ni hatari kuamini uzoefu wangu katika jambo fulani unaweza kutumika katika mazingira mengine kwa mtu mwingine. Tunapokuwa na watu wanaozungumza mambo yenye mwelekeo wa 'saikolojia' katika kujaribu kujibu matatizo ya jamii lakini yasiyokuwa na msingi wa kanuni halisi za saikolojia kisayansi, athari zake zaweza kuwa kubwa na hatari sana.

Pamoja na changamoto hizo, bado ni wazi kuwa elimu hii ikitolewa ipasavyo, na watu wenye uelewa sahihi, changamoto nyingi katika jamii zenye asili yake katika tabia, mitazamo na imani hasi zinaweza kutatuliwa na hivyo watu kuwa na fursa ya kujiletea maendeleo yao.

No comments:

Post a Comment