Tuesday 19 April 2016

KULALA KWENYE MWANGA WA TAA HUSABABISHA SARATANI


KILA mtu anahitaji kulala na usingizi ni kitu kisichoepukika. Kwa mantiki hiyo, ni vyema tukajua namna bora ya kulala, kwa sababu bila ya kujua jambo hili, tunaweza kujikuta kila siku tunahatarisha afya zetu.
Utafiti wa hivi karibuni umeonesha kuwa wanawake wenye tabia ya kupenda kulala usiku huku wakiwa wamewasha taa chumbani, wako kwenye hatari kubwa ya kupatwa na saratani ya matiti.
Watafiti wamegundua kuwa kulala gizani kwa saa kadhaa huboresha uzalishaji wa kichocheo (hormone) kiitwacho ‘Melatonin’ ambacho kina uwezo wa kuzuia ukuaji na ustawi wa uvimbe wa saratani ya matiti (breast cancer tumour).
Kwa upande mwingine, watafiti wamegundua kuwa ulalaji wa kwenye mwanga wa taa usiku husababisha kushuka kwa kiwango cha uzalishaji wa kichocheo hicho cha ‘Melatonin’ kwenye damu mwilini hivyo kuwa sababu ya ukuaji na ustawi wa chembechembe zinazosababisha uvimbe wa saratani ya kwenye matiti.
Utafiti huu, unatufanya tuone umuhimu wa kupenda kulala gizani kuliko kwenye mwanga wa taa, kama baadhi ya watu wanavyopenda kufanya. Inawezekana pia kulala huku taa ikiwaka ni mazoea yaliyojenga tabia, lakini ili kujiepusha na madhara ya saratani ya matiti ambayo hivi sasa imeanza kuenea kwa kasi nchini, inashauriwa kwa akina mama kuacha tabia hiyo.
Ni kweli kwamba huwezi kujiepusha na saratani ya matiti kwa kulala gizani peke yake, lakini ni vyema kufuata ushauri wa wataalamu wetu ili kuwa salama zaidi. Zingatia pia ulaji sahihi wa vyakula vya asili, kama vile matunda na mboga za majani kwa wingi na kufanya mazoezi.
Vile vile unapaswa kufahamu vyakula hatarishi vya maradhi ya saratani na kujiepusha navyo. Tafiti nyingi zimebainisha vyakula vya kusindika kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha maradhi ya saratani. Ulaji wa mara kwa mara wa vyakula vya kusindika, kama vile nyama za kopo, maharage ya kopo, nyanya za kopo, n.k, vimetajwa kuwa miongoni mwa vyakula vinavyoharibu kinga mwilini.
Orodha hiyo ya vyakula inaendelea pia hadi kwenye vinywaji vyenye ladha za matunda mbalimbali, ambavyo kimsingi huwa vimetengenezwa kwa kuchanganya kemikali, rangi, maji na sukari kwa wingi ili kupata ladha ya juisi waitakayo. Vyote hivi huwa havina faida mwilini zaidi ya kukata kiu na kudhoofisha kinga ya mwili.
Hivyo, wito unatolewa kwa watu wote kujenga kinga ya miili yetu kwa kupendelea kula vyakula asilia na kujiepusha na ulaji wa vyakula ‘ready made’ ili kuipa miili yetu uwezo wa kujikinga wenyewe dhidi ya maradhi mbalimbali, ikiwemo saratani.

No comments:

Post a Comment