Wednesday 20 April 2016

Kama Una Tabia Hii Moja Una Uhakika wa Zaidi ya 90% Wa Kufanikiwa Kwenye Chochote Unachofanya.


Kuna tabia moja muhimu sana ambayo inaonekana kwa watu waliofanikiwa sana kwenye kila nyanja ya maisha. Tabia hii kuna watu wengi wanayo ila hawajajijua na kuanza kuitumia na hata kama huna unaweza kuiendeleza na wewe ukafanikiwa sana kwenye maisha yako. Kabla ya kuiangalia tabia hiyo hebu kwanza tuone tafiti zilizofanywa kudhibitisha uhusiano wa tabia hii na mafanikio.
  Miaka ya 1960 profesa Walter Mischel wa chuo kikuu cha Stanford, alianza kufanya tafiti zilizodumu kwa miaka 40 kuhusiana na tabia hii. Katika utafiti wake aliwahusisha watoto wadogo wenye miaka minne mpaka mitano na kugundua siri moja muhimu kwenye mafanikio ya kazi, biashara, afya na maisha kwa ujumla.
  Utafiti huu ulihusisha pipi tamu iliyotengenezwa kwa asali na mmea ijulikanayo kama marshmallow, pipi hii hupendwa sana na watoto.
Katika utafiti huu kila mtoto aliwekwa kwenye chumba chake mwenyewe na mtafiti alileta pipi hiyo aina ya marshmallow. Aliweka pipi hiyo mbele ya mtoto na kumwambia yeye anaondoka na atarudi baadae. Kama akirudi akakuta mtoto hajala hiyo pipi atamuongezea pipi nyingine, ila akikuta ameshakula hatamwongezea nyingine. Kwa hiyo uchaguzi ulikuwa ni kula moja sasa au kusubiri ule mbili baadae.
  Mtafiti aliondoka kwa dakika kumi na tano. Kuna watoto walikula pipi zao mara moja, wengine walijaribu kujizuia ila wakashindwa na wachache sana waliweza kusubiri wasile pipi zao mpaka mtafiti aliporudi. Majibu ya utafiti huu yalitolewa mwaka 1972, kitu kikubwa cha kushangaza kilitokea miaka 40 baada ya utafiti huu.
marshmallowmarshmallow2
  Watafiti waliendelea kuwafuatilia watoto hawa mwaka hadi mwaka kwa kipindi cha miaka 40. Katika ufuatiliaji iligundulika kwamba watoto waliojizuia kula pipi na kusubiri mtafiti arudi, walikuwa na ufaulu mkubwa darasani, walikuwa na uwezekano mdogo wa kutumia mihadarati na waliweza kukabiliana vizuri na changamoto mbalimbali.
  Kwa miaka 40 ya ufuatiliaji mpaka wanakuwa watu wazima, wale ambao waliweza kusubiri na kutokula pipi walikuwa wamefanikiwa sana ukilinganisha na wenzao walioshindwa kuvumilia. Walikuwa na vipato vizuri, afya njema, familia nzuri na mengine mengi kwenye maisha.
  Katika utafiti huu inaonesha kwamba wale wenye uwezo wa kuvumulia na kuepuka furaha ya haraka ili kupata furaha kubwa zaidi baadae wana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kuliko ambao hawana tabia hiyo.
  Hii ni dhahiri kabisa kwenye maisha yetu ya kila siku, wale ambao wanashindwa kuzuia tamaa zao za kupata furaha ya haraka wanajikuta wanashindwa kufanikiwa sana kwenye maisha.
Kama ukiweza kuepuka tamaa ya kufanya starehe utakuwa na muda mwingi wa kufanya shughuli zako na kuwa na matumizi mazuri ya fedha zako. Kama utaepuka tamaa ya kula vyakula vilivyoandaliwa haraka kama chips utakuwa na afya bora. Kama utaepuka tamaa ya kuangalia tv au movie ambavyo vinakupa starehe ya muda mfupi utakuwa na muda mwingi wa kujifunza vitu vya ziada ambavyo vitakusaidia sana kwenye maisha yako.
  Kwenye maisha ya kila siku tunaona ni jinsi gani watu wenye tamaa ya furaha ya muda mfupi wanavyoharibu maisha yao. Wengi wao wanakuwa wezi, walevi, waasherati na masikini wa muda mrefu.
Je unawezaje kutengeneza tabia hii?
Kama mara nyingi umekuwa ukichagua njia rahisi ya kupata furaha inaonesha kwamba tayari haupo kwenye njia ya kupata mafanikio. Je tabia hii ya kuzuia furaha ya muda mfupi ni ya kuzaliwa? Watoto hao walioweza kujizuia kula pipi walizaliwa na tabia hiyo? Je wewe unawezaje kujifunza tabia hii ili uweze kufanikiwa?
  Kabla ya kujibu maswali haya hebu twende kwenye sehemu ya pili ya utafiti huu ambao una majibu mazuri na ya kushangaza kidogo.
Endelea kusoma tabia hii kwenye KISIMA CHA MAARIFA.

No comments:

Post a Comment