Habari mpenzi msomaji wetu?
Karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutazungumzia
kuhusiana na wivu. Wivu ni nini, ni kitu gani basi mpaka kinapelekea mtu kua na
wivu, nini matokeo ya wivu na namna gani au jinsi gani ya kukabiliana na
wivu.
Wivu ni hali ya kuwa na mtazamo hasi juu ya kitu fulani kwa
mfano unachukia au hufurahii kabisa mandeleo ya mwenzako au mtu mwingine
anafurahia kuona mwenzake au jirani yake akipatwa na matatizo na wakati mwingine
wako watu mpaka wanafurahia misiba ya wenzao.
Wivu ni hisia ambayo imetawala katika jamii zetu na hisia ambayo
inawaumiza watu wengi sana na kuleta athari hasi katika maisha ya mtu mmoja
mpaka jamii kwa ujumla. Zifuatazo ni sababu zinazopelekea mtu kuwa na wivu nazo
ni;
1. Kujiona unastahili kuliko wengine;
Kujiona wewe ndio unastahili kupata kuliko wengine hiyo
inapelekea wivu ukiona mwenzako kapata mafanikio juu ya kitu Fulani unaumia
kweli, unapatwa na hasira kabisa na kupata maumivu ya moyo sababu ni kujiona tu
wewe ndio unastahili kupata kuliko mtu mwingine. Binadamu wote ni sawa na kila
mtu ana haki ya kufanikiwa hivyo hupaswi kujiona kuwa wewe unastahili kupata
zaidi kuliko mwingine na ukiwa na zana hii itakutesa sana sehemu yoyote ile
ulipo ukiwa kazini kwako mwenzako akipandishwa cheo unapatawa wivu na kujiona
kuwa wewe ndio unastahili kuliko wengine. Hivyo kuwa huru na furahia mafanikio
ya wenzako na jifunze kupitia wenzako waliofanikiwa badala ya kuonea wivu watu.
SOMA; Huyu Ndiye Mtu Anayekuzuia Kufikia Mafanikio Makubwa, Na Jinsi Ya
Kumshindwa.
2. Kutojiamini;
Kutojiamini ni hali ya kujidharau wewe mwenyewe, hali ya
kutojiamini inapelekea wivu sehemu mbalimbali. Kwa mfano mfanyakazi anamuonea
wivu mfanyakazi mwenzake kwa sababu ya mwenzake anafanya kazi kwa juhudi na
maarifa na kuongeza thamani katika kampuni au taasisi yake. Badala ya mfanyakazi
mwenzake kuiga mazuri au kujifunza mazuri kutoka kwa mwenzake anaanza kumuonea
wivu. Kutojiamini inampelekea kujiona yeye hawezi kuleta mabadiliko katika
kampuni au taasisi yake wakati ana kila sababu ya kuwa bora kama mwenzake hivyo
basi, hali hii inampelekea mtu wa kutojiamini kuwa na wivu na mwenzake. Wapo
watu wengine hawajiamini katika nyadhifa walizonazo au nafasi walizonazo na
kupelekea hali ya wivu hata kudiriki kumwendea mwenzake kwa mganga ili aendelee
kubaki katika nyadhifa au nafasi aliyopo. Kutojiamini, kutokubali mabadiliko
yanayotokea na kutokujifunza zaidi katika taaluma yako na kufanya kazi kwa
mazoea bila ubora wowote inapelekea migogoro ya wivu na madhara ya wivu ni
makubwa sana katika jamii.
3. Kuishi au Kuzungukwa na Watu Hasi;
Kila mtu ana uamuzi wa kuishi maisha anayotaka au
aliyojichagulia hivyo kama wewe umezungukwa na watu chanya katika maisha yako
uko sehemu nzuri sana ya kufikia mafanikio makubwa. Lakini kama wewe umezungukwa
au unaishi na watu hasi upo sehemu mbaya na ya hatari sana. Kuzungukwa na watu
hasi ni kama vile kuwa na marafiki, ndugu, majirani wenye mtazamo hasi hata
kuzungukwa na watu hasi katika mitandao ya kijamii inapelekea hali ya mtu kuwa
na wivu unakuta mtu ameambatana na watu hasi katika mitandao ya kijamii yeye
kila siku ni kuingiza umbea, majungu, katika akili yake hali hii inapelekea
kujenga dhana ya wivu.
SOMA; Kama Unajibebesha Mizigo Hii Katika Maisha Yako, Sahau Kuhusu
Mafanikio.
Matokeo ya kuwa na wivu ni kama ifuatavyo;
i. Kukosa upendo na watu wengine
ii. Kutopenda kuona watu wakifurahi
iii. Kuishi na nyuso za huzuni
iv. Kukosa furaha
v. Kupata majeraha ya moyo
vi. Kuishi maisha ya chuki
vii. Kuishi maisha ya kutokuwa na amani
viii. Huleta mauti
ix. Huleta msongo wa mawazo
x. Kudhoofika kiafya, kama vile kimwili, kiakili na
kiroho.
Namna gani au jinsi unaweza kukabiliana na wivu?
Unaweza kukabiliana na wivu kwa kutumia njia zifutazo nazo
ni;
i. Usijilinganishe Na Mtu Mwingine;
Matatizo ya wivu huanza pale mtu unapoanza kujilinganisha na mtu
mwingine. Unajidharau na kujiona maisha yako unayoishi hayana maana na kuona
maisha ya mwenzako ndio bora kwa njia hii lazima itakupelekea kwenye wivu tu.
Utatamani kitu ambacho hakipo ndani ya uwezo wako matokeo yake mawazo hasi ya
yatakutawala na kupelekea hisia za hasira na hatimaye kuwa na wivu. Hii ni dawa
namba moja ya kuepukana na wivu usijilinganishe na mtu mwingine na ishi maisha
yako.
SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Sumaku Ya Fedha, Njia Kumi (10) Za Kuivuta
Fedha Ije Kwako Muda Wote.
ii. Usimdharau Mtu Mwingine;
Kila binadamu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Hivyo basi
huna haki ya kumhukumu mtu mwingine na kumdharau kulingana na rangi, jinsia,
jinsi, maumbile yake na hata ulemavu wowote ule. Mwenye haki ya kuhukumu si wewe
bali ni Mungu acha mara moja tabia ya kuhukumu na kudharau wengine. Kama
binadamu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu basi ukimdharau mtu mwenzako
utakuwa umemdharau aliyemuumbwa. Hakuna aliyeandika barua ya kuomba kuzaliwa na
azaliwe na namna gani bali wote tunatakiwa kujipokea kama tulivyozaliwa na wala
tusiwadharau watu wengine.
Makala hii imeandikwa na Michael Charles Chali ambaye ni mwanafunzi
mwandishi kutoka Chuo Cha Uandishi wa habari (Dsj), mhamasishaji na mjasiriamali,unaweza kuwasiliana naye kupitia namba
0712562397 au kwa barua pepe micha.connect2015@gmail.com
No comments:
Post a Comment