Tuesday 19 April 2016

HIVI NDIVYO KILA KIZURI HUGEUKA NA KUWA KIBAYA


Natumaini kabisa kwamba kila mtu ana matumizi yake katika maisha yake. Kila mtu hutumia pesa kwa jinsi anavyopenda, kila mtu hutumia usafiri wake kwa jinsi anavyopenda, kila mtu hutumia zana au vitu anavyomiliki kwa jinsi anavyopenda.
Hebu angalia matumizi yako kwa ujumla na ulinganishe na jinsi watu wanavyochukulia matumizi hayo. Je ni mazuri? Au yana walakini? Na kwanini yasiwe mazuri? Je upande wako unayaona mazuri?
Ukweli ni kwamba kila mtu ni mwalimu hivi sasa. Hakuna anayejua zaidi, sote huishi kwa kutaka ushauri baina yetu, Lakini kikubwa ambacho napenda kuzungumzia hapa ni vile utumiaji wako ukafanya kitu unachokitumia kuharibika sifa yake na kuwa sifa mbaya ambayo ikachukiwa na watu.
Hii sana sana hutokea pale mtu anapoweka kitu au jambo katika sehemu isiyo ya kwake au sehemu isiyohusika, sote tunajua kwamba uchafu ni kitu ambacho hakifai katika matumizi ya mwanadamu na mafikio yake ni kutupwa jalalani, Lakini uchafu pia siyo tu kitu kisichofaa katika matumizi ya mwanadamu, bali hata kitu kukaa sehemu isiyohusika pia ni uchafu.
Chukua sahani ya chakula halafu iweke chooni. Hapo mtu akiingia hatoona kuwa choo ndiyo kichafu, bali ataona kuwa chakula ndiyo kichafu. Au weka kikombe au ndoo ya maji katikati ya mlango aidha wa chumbani au sebuleni. Hapo kikombe au ndoo itakuwa ni uchafu kwani uko sehemu isiyohusika ingawa bado kinafaa katika matumizi.
Sasa je unafahamu ya kwamba kila utakayemuuliza maana ya kelele atakujibu kuwa ni ile sauti kali ya juu? Lakini hii ni kweli? Inaweza ikawa kweli kwa baadhi ya sehemu na ikawa ni uwongo kwa baadhi ya sehemu.
Lakini uhakika hasa wa kelele ni ile sauti isiyoeleweka au kuleta maana au mtazamo fulani wenye kutafsirika akilini. Kwa mfano chagua maneno manne mazuri kabisa kama vile dhahabu, gari, fedha na chakula halafu chukua watu wa nne na kila mmoja mpe neno lake kisha uwaambie watamke kwa pamoja. Hapo utaona jinsi utakavyokosa faraja masikioni kwani utaona kama vurugu katika akili kwa maneno tofauti kutamkwa kwa wakati mmoja.
Lakini kama wote watatamka neno moja tu kwa pamoja hapo hutaona tabu wala hutahisi kukosa faraja katika masikio yako hata kama watatamka kwa sauti kubwa.
Kuepukana na yote haya kutatokea ikiwa utakuwa na mpangilio mzuri katika vitu na matumizi yako na kutumia kitu kama kilivyoelekezwa. Lakini kinyume na hapo itakuwa na uchafuzi na uharibifu. Kama mzazi ataamua kumnunulia mwanawe computer games au Playstation game kisha huyo mtoto akawa anaicheza hiyo game halafu ukifika muda wa shule anaenda, ukifika muda wake wa kujisomea anajisomea na mtihani anafaulu vizuri, basi hutamsikia mzazi hata siku moja akisema vibaya au kupinga matumizi ya game kwani imetumiwa vizuri.
Hivyo ningependa kusema kwamba, kaa chini halafu orodhesha vitu unvyojua vinapingwa sana kisha angalia sababu kubwa utaona kuwa ni vizuri tu na vimetengenezwa kwa nia nzuri tu, Lakini sifa yake imekuwa mbaya kutokana na watumiaji wanavyovitumia.

No comments:

Post a Comment