Wednesday 20 April 2016

Kama Unatafuta Kazi,..Haya Ndiyo Mambo Muhimu Ya Kukusaidia Kupata Kazi hiyo.


Wengi wetu mara tunapomaliza masomo huwa tunatafuta ajira kwa njia mbalimbali. Kuna wakati tunaandika barua za maombi na kusubiri, kuna wakati tunasaidiwa na jamaa zetu kupata ajira na kuna wakati tunapita ofisi moja hadi nyingine kuomba ajira.
Katika kutafuta ajira, kama ilivyo katika shughuli nyingine, kuna kanuni. Hebu  tuchukulie wewe ni  kijana na ndiyo kwanza umemaliza masomo yako ya chuo na umeenda kwenye usaili (Interview) kwa ajiri ya kupata ajira. Unafikiri hasa ni mambo gani ambayo unatakiwa kufanya?
Hebu tuanze na kujiamini. Hakuna kitu utakachosema wakati wa usaili kinachoweza kuwa na umuhimu kama mwenyewe hutaonekana mtu mwenye kuaminika. Kiongozi wako mpya wa kazi ni lazima akuamini. Hakuna mtu aliyetayari kuajiri mtu ambaye anajua hatomwamini. Sasa ni vipi utajenga kuaminika?
Kwanza ni muhimu uzungumze ukweli. Wapo watu wenye uwezo wa kuongopa vizuri sana na wasigundulike. Lakini hawa ni wachache sana. Wengi wetu huweza kujikuta tukigundulika kwamba hatusemi ukweli.
Unajua jinsi ambavyo hata wewe mwenyewe umewahi kuzungumza na mtu na kuhisi kwamba anachokueleza si ukweli. Hilo ni tatizo la wengi wetu na wala usidhani ni tatizo la huyu mtu aliyekuwa akikueleza wewe tu.
Kama unajiamini na unaamini ukweli wa kile unachosema. Hata uwe mtu mwenye tabia ya wasiwasi kiasi gani, hali ya uwazi na usahihi wa mazungumzo yako itaonekana wazi.
Pili, unatakiwa kuwatazama machoni unaozungumza nao. Huna haja ya kuishangaa miguu yao, ama kushangaa kikombe kilichowekewa kalamu juu ya meza ya msaili wako au kushangaa feni iliyo kwenye dari la chumba cha usaili
Fanya kila jitihada umtazame moja kwa moja msaili au wasaili na uzungumze katika hali ya kawaida iwezekanavyo. Hakutakuwa na  tatizo kuwatazama machoni wakati unapeana mikono na kuwaeleza, ‘samahani, kidogo mimi mimi nina tatizo la kukumbwa na wasiwasi kirahisi’. Kama ni msaili au wasaili ni wenye busara, ni lazima watazungumza kitu chenye lengo la kukutoa wasiwasi.
Lakini ikiwa msaili ataonesha kukudharau kwa kauli yako hiyo ya ukweli, basi kuwa na uhakika kwamba hata ukipata nafasi unayotaka hutofurahia kufanya naye kazi.
Unataka kumvutia mkuu wako mtarajiwa wa kazi pamoja na wafanyakazi wenzako, kama vile wewe unavyopenda majukumu yako. Hivyo, kuwa wazi na mwaminifu katika kipindi chote cha usaili, na kumbuka kwamba unayo nafasi ya kuwasaili wao pia kama wakuu wako wa baadaye wa kazi, na wala si jambo la upande mmoja. Kama ilivyo kwako, nawe unatakiwa kuwa na hakika kama utafanya nao kazi vizuri.
Hebu sasa tutazame picha kwa ujumla ya namna unavyoweza kujtafutia soko na kujitambulisha kama mtu mwenye uwezo wa kazi, mwenye uwezo wa kutegemewa, mwenye akili, mwaminifu na rasilimali nzuri za baadaye  kwa kampuni.
Kwanza, huwezi kuanza kuomba kazi, bila kujiamini kwamba una vitu vyote hivyo. Mkesha wa siku ya usaili, pitia mambo yote muhimu ambayo mkuu wako wa kazi angepennda uwe nayo kama mfanya kazi wake.
Chukua nafasi ya mkuu wako huyo wa kazi akilini mwako na ufikirie kama ungekuwa wewe ni vitu gani ungetafuta kama mfanyakazi wako mpya. Unaweza kufanya majaribio ya usaili na ukiweza, mpate rafiki yako atakayekusaidia kufanya hivyo.
Unaweza kujiuliza maswali yafuatayo…Nina uwezo? Ninao utaalamu wa msingi unaotakiwa ili kuweza kuifanya kazi hii ama nahitaji mafunzo zaidi? Ni vipi nitaweza kujifunza kwa haraka.
Haitakuwa vibaya sana kwako kama ukienda zaidi ya uwezo wako wa sasa na kujaribu kutazama mambo yanayoweza kuwa changamoto. Lakini unatakiwa kuwa mwaminifu na huna haja ya kujidai tayari unaweza kila kitu, kwa kiwango cha juu kabisa, wakati una hakika si hivyo.
Endelea na orodha ya maswali…Je wewe ni mtu wa kutumainiwa? Ni uwezo upi mpya mbali na yale uliyoorodhesha kwenye orodha ya mahitaji ya kazi utakaouleta kwenye kampuni? Uwe tayari kumweleza msaili wako mambo ya ziada ambayo kampuni itafaidika nayo ikiwa itakuajiri.
Rudia majibu yajo kwa msaili wako wa kufikirika, ili utakapoingia kwenye chumba cha usaili uwe tayari na mawazo ya kile utakachomweleza msaili wako ili kujitafutia soko vizuri.
Kwa kuwa na majibu yako yaliyotayarishwa, utakuwa na wakati rahisi wa kujitambulisha kama mtu mwenye busara na akili hata kama una kawaida ya kuogopa sana pale usaili wa kweli unapoanza.

SOMA; Dalili 8 Za Kutofanikiwa Kwa Kile Unachofanya.

Mwisho, usijaribu hata siku moja kuonyesha kutokujiamini. Wahi muda uliopangwa, vaa nguo zinazohitajika kwa ajili ya kazi uliyoomba, jua jina la kampuni unayoomba kazi, kazi unayoomba, na mfahamu anayekusaili.
Ni vema ukawahi na kujua zilipo huduma nyingine za muhimu kama choo, bafu na kadhalika. Huna haja ya kulijaza tumbo lako na vitu vya majimaj ama chakula.
Baadhi ya mambo haya yaweza kuonekana ya kijinga, lakini hakuna kitu kibaya kama kuonekana ukihangaika kwenye kiti ulichoketi kutokana na usumbufu wa tumbo ama kibofu chako cha mkojo, wakati unatakiwa kuonekana mwenye kujiamini, uliyetulia na uliyetayari kwa usaili.
Kuwa macho na namna unavyozungumza. Epuka kutumia maneno makali na lugha ya mtaani. Kuwa macho na lafudhi. Usiruhusu lafudhi ya ajabu au sauti iliyosikia ikufanye ukose kazi uliyokuwa ukiitoa siku zote.
Kumtumia rafiki yako kwa usaili wa majaribio, kwa weza kukusaidia kuongeza sana kujiamini wakati msaili wako wa kweli atakapokuwa mbele yako. Kama kweli unajiamini, kujitafutia soko hakuwezi kuwa jambo gumu. Fanya mazoezi kwa kile unachotaka kukisema.
Kama kweli hujiamini, basi ni bora ukafanya jitihada za kuondoa tatizo hilo kwanza. Kama lengo ni kujijengea maisha mazuri na ya furaha, basi iko haja ya wewe nawe kuwasaili wanaotaka kukuajiri ili kujua kama watafaa kukujengea maisha hayo ya furaha baadaye. Unatafuta mwajiri aliyetulia na rahisi kufanya naye kazi.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi kila siku.
Tunakutakia kila la kheri katika mafanikio ya kazi unayoitafuta.
Ni wako rafiki katika mafanikio,

No comments:

Post a Comment